Dodoma FM

Dodoma yabainisha watoto wenye mahitaji maalum

22 January 2026, 5:25 pm

Picha ni baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum jijini Dodoma. Picha na Wilaya ya Dodoma.

Ubainishaji wa mapema utasaidia serikali na wadau kupanga mikakati madhubuti ya utoaji wa huduma kwa watoto wenye mahitaji maalum.

Na Lilian Leopold.

Wazazi na walimu wametakiwa kushirikiana katika kuwaibua watoto wenye mahitaji maalum, kwa lengo la kuwatambua watoto hao wenye changamoto mbalimbali za kiafya na kielimu ili waweze kupata huduma stahiki.

Akizungumza katika hafla ya kuwatambua watoto wenye mahitaji maalum Naibu Meya wa jiji la Dodoma , Bakari Fundikira amesema zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya serikali ya kuhakikisha watoto wote wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu, afya na ustawi wa kijamii bila ubaguzi.

Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Jiji la Dodoma, Joseph Fungo amesema Jiji la Dodoma litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanahudumiwa ipasavyo

Picha ni baadhi ya watoto wenye mahitaji maalum wakiwa na wazazi wao. Picha na Wilaya ya Dodoma.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuacha kuwaficha watoto wenye changamoto, akisisitiza kuwa jamii ina wajibu wa kupinga unyanyapaa na mitazamo hasi dhidi ya watoto wenye mahitaji maalum.

Zoezi la ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum linatarajiwa kufanyika katika kata mbalimbali za jiji la Dodoma, likiwa na lengo la kuwafikia watoto wengi zaidi na kuhakikisha hakuna mtoto anayeachwa nyuma.