Dodoma FM
Dodoma FM
21 January 2026, 1:52 pm

Aidha, utafiti huo unaeleza kuwa ingawa 41.3% ya kaya hutumia mbegu bora, 79.6% bado hutegemea mbegu za asili, hali inayochangia kiwango kidogo cha tija.
Na Lilian Leopold.
Wakulima jijini Dodoma wametakiwa kuzingatia njia sahihi za uandaaji wa shamba, ikiwemo kupima udongo, kusafisha shamba mapema na kuongeza mbolea ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Wito huo umetolewa wakati ambapo Utafiti wa Mwaka wa Sampuli za Kilimo (AASS) 2022/23 unaonesha kuwa kilimo bado ni mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, kikihusisha kaya milioni 8.97, ambapo 98.3%huzalisha mazao na 60.6% hufuga mifugo.Hata hivyo, ni asilimia 4.6 tu ya ardhi inayolimwa, sawa na hekta 922,852, inayomwagiliwa, hali inayowafanya wakulima wengi kutegemea mvua na kuwa katika hatari ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na Taswira ya habari, Mtaalam wa masuala ya kilimo Jofrey Samwel kutoka Kampuni ya Josasa Farms iliyopo Nzuguni, amewasisitiza wakulima kuanza maandalizi ya mashamba yao mapema kabla ya msimu wa kilimo na kuachana na mbinu za kilimo cha mazoea.

Kwa upande wake Ally Mnyasi, mkulima wa mbogamboga na nafaka kutoka Nzuguni eneo la Nanenane, amesema matumizi ya njia sahihi za uandaaji wa shamba yamechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzaishaji wa mazao yake ikilinganishwa na awali alipokua akitegemea kilimo cha mazoea.
Sera ya Kilimo ya Taifa ya Tanzania (2013)inalenga kubadilisha kilimo kutoka mfumo wa mazoea wa jadi kwenda kilimo cha kisasa, tija na biashara. Sera hii inaweka msisitizo katika mabadiliko ya sekta ya kilimo kwa kuweka malengo makuu ya kuibua kilimo cha kisasa kinachoweza kuchangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa wakulima.