Dodoma FM
Dodoma FM
16 January 2026, 12:05 pm

Zoezi hilo ni sehemu ya kampeni kubwa ya serikali ya kuikijanisha Dodoma kwa kupanda miti.
Na Lilian Leopold.
Katika jitihada za kuufanya mkoa wa Dodoma kuwa wa kijani na kustawisha mazingira, zoezi la ugawaji wa miche ya matunda na kivuli limefanyika katika kata ya Nala, Shule ya sekondari Nala mkoani Dodoma, ambapo miche 2,900 imetolewa kwa wananchi wa mitaa yote sita ya kata hiyo.
Zoezi hilo limehudhuriwa na watumishi wa kanda namba tatu, Diwani wa kata ya Nala na wananchi waliojitokeza kupata miche hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani wa kata ya Nala, Leonard Malima amesema kampeni ya kuikijanisha Dodom itaendeshwa kikamilifu katika kata hiyo na kusisitiza kwamba wale wote waliopewa miche watatembeewa mara kwa mara ili kufuatilia utunzaji wa miti hiyo.

Kwa upande wake Mhandisi wa Kanda namba tatu, Joha Ntonga amesema zoezi la upandaji wa miti ni zoezi endelevu kwani lina faida kubwa kwa jamii.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Nala waliojitokeza kupata miche hiyo akiwemo Stanley Msaga na Zena Noel wamesema wamefurahishwa na zoezi hilo, huku wakiongeza kuwa bado wana uhitaji na miche.

Kampeni ya upandaji miti mkoani Dodoma imekuwa ikiendeshwa tangu mwaka 2024, ikijulikana kama kampeni ya “Mti wangu, Birthday yangu”, iliyozinduliwa rasmi tarehe 18 Oktoba 2024na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.