Dodoma FM
Dodoma FM
15 January 2026, 12:35 pm

Amewataka viongozi katika sekta ya afya kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za huduma bila kusubiri michakato mirefu.
Na Mariam Kasawa
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Seif Shekalaghe, kufanya mapitio ya miongozo ya afya na marekebisho ya kanuni ili mabaraza ya wataalamu wa afya washughulikie watoa huduma wanaosababisha vifo vya mama mjamzito na mtoto kwa uzembe.
Kauli hiyo imetolewa leo wakati wa kikao kazi na watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya na watumishi wa sekta ya afya, kilichofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), jijini Dodoma.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amewataka viongozi katika sekta ya afya kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za huduma bila kusubiri michakato mirefu inayosababisha kukwama kwa maamuzi na kuwaacha wagonjwa wakikosa huduma muhimu kwa wakati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika upanuzi wa huduma za kibingwa na ubingwa wa juu ndani ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Prof. Makubi amefafanua kuwa hadi kufikia tarehe 13 Januari 2026, hospitali hiyo inatoa huduma kwa kutumia jumla ya watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa wa juu 100 na wauguzi 400. Ameongeza kuwa kwa idadi hiyo na huduma zilizoboreshwa, hospitali ya Benjamin Mkapa imeendelea kuweka alama kubwa katika mapinduzi ya tiba nchini.