Dodoma FM
Dodoma FM
14 January 2026, 5:52 pm

Mazungumzo hayo yanaonesha dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kushirikiana na wadau wa kimataifa katika kufanikisha vipaumbele vya maendeleo ya taifa na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji kwa ajili ya ustawi wa jamii na uchumi wa nchi.
Na Mwandishi wetu.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), amesema ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Jamhuri ya Korea utaimarisha huduma ya majitaka kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.
Waziri Aweso amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania, Mhe. Ahn Eunju kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo katika Sekta ya Maji kwa kutekleza miradi mbalimbali ya maji nchini.
Waziri Aweso amesema Serikali ya Tanzania na Korea zinashirikiana katika kutekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Huduma ya Usafi wa Mazingira katika Jiji la Dar es Salaam wenye thamani ya takribani Dola za kimarekani milioni 90 unaotarajiwa kuwanufaisha wananchi wanaokadiriwa kufikia milioni 1.8 katika jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA).
Mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, yalijikita katika masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, hususan katika maeneo ya kuimarisha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira, rasilimali za maji na usalama wa maji, majitaka, uvunaji wa maji ya mvua pamoja na fursa za uwekezaji katika Sekta ya Maji.

Amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Kinondoni ndiyo maeneo ambapo mradi huo mkubwa unatekelezwa na mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 10.8, utasaidia kuboresha mfumo wa majitaka yanayozalishwa baada ya matumizi ya majisafi ambayo yanatarajiwa kuongezeka.
Kupitia utekelezaji wa mradi wa kisasa wa uondoshaji majitaka kwa ujenzi Mtambo wa Kisasa wa Kuchakata Majitaka eneo la Buguruni (maarufu Mabwawa ya Majitaka Buguruni) na kuachana mfumo wa zamani wa kuchakata majitaka kwa kutumia mabwawa ambayo yamejengwa karibu kabisa na eneo la makazi ya Buguruni Jijini Dar es Salaam. Mradi huu unatarajiwa kumaliza magonjwa ya mlipuko yalliyokuwa yanawakabili wananchi wa maeneo hayo na kupunguza gharama za uondoshaji wa majitaka kwa wananchi haswa katikati ya Jiji la Dar es salaam.
Aidha, mazungumzo hayo yameangalia ushirikiano katika fursa mpya ikiwa ni pamoja na Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria kufika Dodoma na Maji ya Mto Rufiji kufika Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha huduma ya maji katika majiji hayo.
Kwa upande wake, Balozi Ahn Eunju amempongeza Waziri Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta ya Maji pamoja na kufurahishwa na kazi ya utekelezaji wa Mradi wa Majitaka Buguruni.
Balozi Eunju amesisitiza dhamira ya Korea kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya usalama wa maji ni eneo muhimu la ushirikiano, hususan katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la mahitaji ya huduma za maji.