Dodoma FM
Dodoma FM
13 January 2026, 2:33 pm

Kwa mujibu wa utafiti wa Demographic and Health Survey (DHS), kiwango cha uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi nchini Tanzania bado ni kidogo, ambapo ni takribani asilimia 7 tu ya wanawake ndiyo wamewahi kupimwa, hali iliyo chini ya lengo la WHO la kufikia angalau asilimia 70 ifikapo mwaka 2030.
Na Lilian Leopold.
Saratani ya shingo ya kizazi imeendelea kuwa tishio kubwa kwa wanawake nchini Tanzania, huku wataalam wa afya wakieleza kuwa baadhi ya mila na desturi zinazohusisha kuozesha mabinti wakiwa wadogo zinaweza kuongeza hatari ya maambukizi.
Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO), tafiti za kisayansi na taarifa za afya kwa umma, takwimu za mwaka 2024 zinaonesha kuwa saratani imeendelea kuwa tatizo kubwa la kiafya, takribani wanawake 10,000 hadi 10, 241 hupata ugonjwa huu kila mwaka huku vifo vikikadiriwa kuwa 6,500 hadi 6,800.
Dkt. Magreth John, daktari wa magonjwa ya binadamu kutoka jijini Dodoma ameelezea kuwa mila zinazokubali kuozesha binti akiwa na umri mdogo zinachangia kuongezeka kwa maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi.
Aidha Dkt. Magreth amebainisha makundi ya wanawake walio hatarini zaidi kupata saratani, ikiwemo wanawake walioanza kufanya ngono mapema, wale wenye wapenzi wengi na wale wenye kinga dhaifu.
Kwa upande wake Dkt. Innocent Kitandu, pia daktari wa magonjwa ya binadamu ameongeza kuwa saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na kirusi aina ya HPV (Human Papillomavirus), huku akibainisha dalili za ugonjwa huu.
Nao baadhi ya wanafunzi wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma wameitaka jamii kuachana na mitazamo hasi hususani kuhusu chanjo ya HPV na badala yake kuunga mkono juhudi za kinga kwa wasichana.