Dodoma FM

Wakuu wa shule watakiwa kuepuka ucheleweshaji wa masomo

12 January 2026, 1:26 pm

Picha ni Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma, Mwalimu Prisca Myalla wakati akizungumza na walimu. Picha na Dodoma City Tv.

Kauli hiyo inatokana na Waraka wa Elimu Na. 05 wa mwaka 2025 na Waraka wa Elimu Na. 06 wa mwaka 2025, ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeeleza rasmi ratiba ya muhula wa masomo kwa shule za awali, msingi na sekondari kwa mwaka 2026. Kwa mujibu wa kalenda hiyo, shule zote nchini zinatarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 13 Januari, 2026.

Na Lilian Leopold.

Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kufunguliwa kwa shule nchini, wakuu wa shule jijini Dodoma wametakiwa kuhakikisha kuwa zoezi la kuanza masomo linaanza mara moja bila kuchelewa, pindi shule zitakapofunguliwa rasmi Januari 13, 2026.

Wito huo umetolewa na Mwalimu Prisca Myalla, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma, wakati akizungumza na walimu jijini humo, akisisitiza kuwa ni wajibu wa walimu wote kuwepo shuleni mapema na kuanza utekelezaji wa ratiba ya masomo mara moja ili kuhakikisha muda wote wa muhula unatumika ipasavyo.

Mwalimu Myalla amesema kuchelewa kuanza masomo husababisha upotevu wa muda na kuathiri utekelezaji wa mitaala, hali inayoweza kudhoofisha ubora wa elimu kwa wanafunzi.

Sauti ya Prisca Myalla.
Picha ni baadhi ya walimu waliojitokeza kuzungumza na Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Jiji la Dodoma, Mwalimu Prisca Myalla. Picha na Dodoma City TV.

Akihitimisha, Mwalimu Myalla amewataka wakuu wa shule na walimu kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha mazingira rafiki ya kujifunzia yanaandaliwa mapema, huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanafunzi wanaripoti shuleni kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa mwanzo wa muhula.