Dodoma FM
Dodoma FM
9 January 2026, 3:31 pm

Ameeleza kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakipata hasara kutokana na makosa ya kulima bila kutifua ardhi, kutotumia mbegu bora na kupanda bila kufuata kanuni za kitaalamu.
Na Anwary Shabani.
Wakulima wametakiwa kutambua ukanda wa kilimo wanaoishi ili kufanya maandalizi sahihi ya kilimo na kupanda mbegu zinazoendana na mazingira ya eneo husika, hatua itakayosaidia kuepuka hasara na kuongeza mavuno mengi na bora.
Wito huo umetolewa na Justina Munisi, Afisa Kilimo Mstaafu wa Jiji la Dodoma, wakati akizungumza na Taswira ya habari ambapo amesema ni muhimu wakulima kuzingatia kanuni za kitaalamu katika shughuli za kilimo.
Amesema kuwa Tanzania ina ukanda mbalimbali wa kilimo, hivyo si kila zao linaweza kustawi katika kila eneo, jambo linalowalazimu wakulima kujua aina ya udongo, hali ya hewa na mbegu zinazofaa katika maeneo wanayoishi.
Aidhaa, Justina Munisi amebainisha kuwa ili wakulima wapate mavuno mengi na yenye ubora, wanapaswa kuzingatia nafasi sahihi kati ya mche mmoja na mwingine pamoja na matumizi ya mbegu bora zilizo thibitishwa kitaalamu.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima katika Jiji la Dodoma wamesema kuwa wamekuwa wakifanya maandalizi mbalimbali kabla ya msimu wa kilimo ikiwemo kuandaa mashamba mapema, kuchunguza ubora wa mbegu pamoja na kuzingatia muda sahihi wa kupanda ili kuepuka hasara na kuongeza uzalishaji.
Sanjari na hayo, bi.Justina Munisi amewashauri wakulima kuwatumia maafisa kilimo waliopo katika kata na mitaa yao ili kupata elimu sahihi ya kilimo, hatua itakayosaidia kuongeza kipato na kuondokana na umaskini.