Dodoma FM
Dodoma FM
9 January 2026, 2:41 pm

Picha ni baadhi ya wananchi waliojitokeza halmashauri ya jiji la Dodoma kuchukua namba kwa ajili ya malipo ya viwanja. Picha na Lilian Leopold.
Hatua hiyo inatekelezwa kufuatia notisi ya siku 21 iliyotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuanzia tarehe 30 Desemba 2025 kwa wadaiwa wa malipo ya viwanja katika maeneo ya Mtumba Zone II, Mtumba Zone III na Kikombo, ikiwataka kukamilisha malipo yao kabla ya viwanja hivyo kuchukuliwa hatua ya kuuzwa.
Na Lilian Leopold.
Wananchi jijini Dodoma wameeleza kuridhishwa na huduma zinazotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma, hususan huduma ya upatikanaji wa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya kulipia viwanja, wakisema utaratibu uliowekwa umeongeza ufanisi na kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata namba za malipo wameeleza kuwa utaratibu uliowekwa ni rafiki na unaokoa muda, huku wakitoa wito kwa wadaiwa wengine kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hiyo na kuepuka hatua za kisheria.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini jiji la Dodoma, Dennis Gondwe amesema kuwa siku ya Jumamosi tarehe 10 Januari 2026, wadaiwa wa viwanja wanatakiwa kufika katika duka la kuuzia viwanja kwa ajili ya kupata namba ya malipo (control number).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Gondwe tarehe 29 Desemba 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari, viwanja vyenye thamani ya shilingi bilioni 55.4 bado havijalipiwa. Kati ya hivyo, wadaiwa wa Mtumba Zone II wanadaiwa shilingi bilioni 28.8, Mtumba Zone III shilingi bilioni 20.6, huku eneo la Kikombo likiwa na deni la shilingi bilioni 5.9.