Dodoma FM
Dodoma FM
8 January 2026, 4:04 pm

Baadhi ya wadau waliojitokeza katika hafla ya utiaji saini hati za makubaliano ya ushirikiano katika Chuo Kikuu cha Dodoma jijini Dodoma na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Shirika la Legal Services Facility (LSF). Picha na Anwary Shabani.
Makubaliano hayo yametiwa saini leo jijini Dodoma, ambapo yanalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa sheria na kupeleka huduma za kisheria karibu zaidi na wananchi, hususan wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Na Anwary Shabani.
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetia saini hati za makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Shirika la Legal Services Facility (LSF) kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi, hususan makundi maalumu.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Profesa Razack Bakari Lokina, amesema ushirikiano huo utaongeza uwezo wa UDOM kuzalisha na kutumia wataalamu wa sheria kuwafikia wananchi wengi kwa haraka zaidi, hasa walioko katika mazingira magumu ya kufikia haki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Bi. Lulu Ng’wanakilala, amesema ajenda kuu ya shirika hilo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya kisheria bila vikwazo, akisisitiza kuwa kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na UDOM, wanaamini wataweza kusaidia eneo kubwa la nchi kwa ufanisi zaidi.

Picha ni baadhi ya wadau waliojitokeza katika hafla ya utiaji saini hati za makubaliano ya ushirikiano katika Chuo Kikuu cha Dodoma jijini Dodoma. Picha na Anwary Shabani.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim C. Mwasi, amesema wananchi wengi hushindwa kufikia mifumo ya haki kutokana na uhaba wa wanasheria, na kuitaka Chuo Kikuu cha Dodoma kufungua kituo cha huduma za kisheria cha mkoa kitakachosaidia kutoa ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani.
Kwa ujumla, makubaliano haya yanatarajiwa kuimarisha haki kwa wananchi kwa njia ya ushirikiano wa kitaasisi, kuongeza wataalamu wa sheria, na kusogeza huduma za kisheria karibu zaidi na jamii.