Dodoma FM

Wataalam Jiji la Dodoma wakagua ujenzi wa vyoo Chiwondo

8 January 2026, 3:01 pm

Picha ni ujenzi wa matundu ya vyoo unaoendelea katika Shule ya Msingi Chiwondo iliyopo Kata ya Nala jijini Dodoma. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Shule hiyo ilitengewa kiasi cha shilingi 17,200,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 18 ya vyoo ambapo mradi huo upo katika hatua za mwisho za umaliziaji ambapo kazi iliyobaki kabla ya kuukabidhi mradi ni kumalizia kuweka milango, kufunika karo na kuweka mfumo wa upatikanaji maji.

Na Mariam Kasawa.

Wataalam Kanda Namba Tatu Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamefanya ziara ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo ambapo walitembelea mradi wa ujenzi matundu 18 ya vyoo katika Shule ya Msingi Chiwondo iliyopo Kata ya Nala jijini Dodoma.

Akizungumza na Timu ya wataalam wa Kanda Namba Tatu, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chiwondo, Mwl. Ally Maandazi amesema kuwa mradi huo utakamilika mapema na kwamba wanafunzi watakaporejea kuanza muhula mpya wa masomo wataanza kuvitumia.

Picha ni Wataalam Kanda Namba Tatu Halmashauri ya Jiji la Dodoma wakifanya ziara ya Ukaguzi wa matundu ya vyoo Shule ya Msingi Chiwondo . Picha na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda Namba Tatu, Christina Changwala ameitaka shule pamoja na mkandarasi kumalizia ujenzi huo haraka ili kuepusha usumbufu kwa wanafunzi kukosa huduma muhimu za kijamii pindi watakaporejea shule zitakapofunguliwa tarehe 13 Januari, 2026.

‎Katika hatua nyingine, Mchumi wa Kanda Namba Tatu, William Mdoya ameeleza kuwa nia ya serikali ni kuboresha mundombinu muhimu katika sekta ya elimu ni kutaka kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma zote stahiki katika mazingira rafiki ili waweze kusoma kwa bidii na hatimae kuzifikia ndoto zao.