Dodoma FM

Wazazi, walezi wasiopeleka watoto shule kuchukuliwa hatua kali

7 January 2026, 4:20 pm

Picha ni Afisa Elimu kata ya Mazae alipokuwa akizungumza na baadhi ya wazazi na walezi  wa watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza. Picha na Steven Noel.

Serikali imesisitiza kuwa kuwapeleka watoto katika ajira, hususan kazi za ndani, ni kosa la kisheria, na itachukua hatua dhidi ya wazazi au walezi watakaokaidi wito wa kuwarejesha watoto shule ili waanze rasmi masomo yao kwa wakati.

Na Steven Noel.

Wazazi na walezi waliowapeleka watoto wao kufanya kazi za ndani katika mikoa mbalimbali wametakiwa kuwarejesha mara moja watoto  hao ili kuanza rasmi msimu wa masomo unaotarajia kuanza Januari 13, 2026.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Elimu kata ya Mazae alipokuwa akizungumza na baadhi ya wazazi na walezi  wa watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza  katika shule za Mwanakianga na Mazae, huku akiongeza kuwa kila mtoto ana haki ya kupata elimu hivyo mzazi atakayeshindwa kumpeleka mtoto shule atachukuliwa hatua kali.

Afisa elimu ameongeza kuwa katika shule ya Mazae ni wanafunzi 206 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2025 lakin wanafunzi 197 ndio waiochaguliwa  kuanza kidato cha kwanza 2026.

Sauti ya Afisa Elimu.
Picha ni Mtendaji wa kijiji cha Idilo Bw. Lucas Lameck akizungumza na wazazi na walezi wa watoto waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza. Picha na Steven Noel.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Idilo Bw. Lucas Lameck  amesema kwa mujibu wa Sheria ya mtoto ya mwaka 2019  ni kinyume cha Sheria na ukatili kumwajili mtoto na malipo kupokea wazazi hivyo ametumia fusa hiyo kuwaasa wazazi na walezi wote kuwarejesha wanafunzi walioenda mikoani kufanya kazi za ndani ili waanze masomo.

Sauti ya Lucas Lameck.

Picha ni mzazi mwenye mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kitado cha kwanza. Picha na Steven Noel.

Mmoja wa wazazi ambae tayari amempeleka mtoto wake kufanya kazi za ndani ameahidi kumrejesha mtoto huyo ili kuanza rasmi masomo yake.

Sauti ya mzazi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2019 pamoja na miongozo ya elimu ya msingi, kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kuhakikisha mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu bila kikwazo chochote.