Dodoma FM
Dodoma FM
7 January 2026, 3:13 pm

Picha ni Zaituni Ally Liyendikiye, Afisa Mradi kutoka Shirika la TAHEA, katika kipindi cha Dodoma Live. Picha na Noah Patrick.
Shirika la TAHEA linaendelea kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana katika kuwawezesha vijana, ili kujenga jamii yenye vijana wenye afya, maarifa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Na Anwary Shabani.
Imeelezwa kuwa elimu sahihi ya afya ya uzazi na stadi za maisha kwa vijana balehe inawasaidia vijana kufanya maamuzi sahihi na kujikwamua kiuchumi.
TAHEA ni shirika lisilo la kiserikali ambalo limejikita katika kutoa elimu ya kiuchumi na afya ya uzazi kwa vijana balehe, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kufanikisha malengo yao ya maisha na kujikwamua kiuchumi katika jamii.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Zaituni Ally Liyendikiye, ambaye ni Afisa Mradi kutoka Shirika la TAHEA, amesema kuwa mradi huo unalenga kuwaandaa vijana rika balehe kwa kuwapatia elimu sahihi ya afya ya uzazi pamoja na stadi za kiuchumi, ili waweze kufanya maamuzi sahihi na kujenga mustakabali wao bila kutegemea wengine.
Zaituni amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, vijana wanawezeshwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujasiriamali, uwekezaji mdogo mdogo na mbinu za kujilinda kiafya, hatua inayosaidia kupunguza changamoto za kiuchumi na kijamii miongoni mwao.
Hata hivyo, afisa huyo amebainisha kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya kuwapata vijana wengi kujiunga na mradi huo, hasa kutokana na baadhi yao kutamani mafanikio ya haraka bila kupitia mchakato wa kupata elimu na mafunzo stahiki.

Kwa upande wao baadhi ya vijana walionufaika na mradi huo wamesema elimu wanayoipata imewasaidia kubadilisha mtazamo wa maisha, na kuanza kufikiria maendeleo ya muda mrefu badala ya kupoteza muda katika mambo yasiyo na tija.
Wamewahimiza vijana wenzao kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na mashirika mbalimbali, wakisema elimu hiyo ni msingi muhimu wa mafanikio yao ya baadaye.