Dodoma FM
Dodoma FM
6 January 2026, 4:46 pm

Picha ni maji machafu ya mvua yaliyotuhama katika baadhi ya makazi ya watu, mtaa wa Miyuji Proper. Picha na Lilian Leopold.
Jamii imetakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kufunika mitaro wazi, kuondoa maji yaliyotuama, kuwafuatilia watoto wanapocheza pamoja na kuwahimiza watoto kuepuka kucheza karibu na madimbwi ya maji.
Na Lilian Leopold.
Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dodoma, zimeibua haja ya wananchi katika kata ya Miyuji mtaa wa Miyuji Proper kuongeza tahadhari katika ulinzi wa watoto, hususan dhidi ya madimbwi ya maji, mitaro na miundombinu isiyo salama.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa hatari zinazotokana na maji yaliyotuama, mitaro wazi na miundombinu isiyo salama, hali inayoweza kusababisha ajali na magonjwa ya mlipuko kwa watoto iwapo tahadhari hazitachukuliwa kwa wakati
Dodoma FM imepita mtaani kuzungumza na baadhi ya wananchi,ambapo wamesema kwa sasa wamekuwa wakihakikisha watoto hawachezi karibu na madimbwi ya maji, mitaro pamoja na maeneo yenye miundombinu chakavu ili kupunguza ajali na hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kwa watoto.
Aidha wameongeza kuwa ulinzi wa watoto si jukumu la mzazi au mlezi pekee, bali ni wajibu wa jamii nzima bila kujali anatoka familia ipi, na kusisitiza umuhimu wa mwanajamii kuwajibika pindi aonapo mtoto yupo katika mazingira hatarishi.
Kwa upande wake Dickson Lazaro Balozi wa shina namba 13 mtaa wa Miyuji Proper amesema kama uongozi wa mtaa wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye miundombinu ya barabara na mitaro, ili kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na kuzuia hatari zinazoweza kuwakumba watoto.
Balozi Dickson amehitimisha kwa kutoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao, kuwapa elimu na kuwazuia kucheza kwenye maeneo hatarishi ili kulinda maisha na afya zao.