Dodoma FM
Dodoma FM
5 January 2026, 4:19 pm

Sera hiyo inasisitiza ushirikiano kati ya serikali, jamii na wazazi katika kuondoa vikwazo vya upatikanaji wa elimu, ikiwemo kuhakikisha watoto wanajiandikisha na kuhudhuria shule ili kupata maarifa na stadi muhimu kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Na Lilian Leopold.
Kuelekea muhula mpya wa masomo utakaoanza rasmi tarehe 13 Januari 2026, wazazi na walezi jijini Dodoma wameonyesha mwitikio chanya katika maandalizi ya kuwarejesha watoto shuleni, wakieleza dhamira ya kuhakikisha watoto wanapata elimu kama ilivyokusudiwa.
Hatua hiyo inakuja kufuatia taarifa iliyotolewa rasmi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tarehe 29 Desemba 2025 kwa umma iliyolenga kukanusha taarifa potofu iliyokuwa ikisambaa mtandaoni ikidai kuwa shule hazitafunguliwa Januari 2026.
Kupitia Waraka wa Elimu Na. 05 wa mwaka 2025 na Waraka wa Elimu Na. 06 wa mwaka 2025 Wizara imeeleza ratiba ya muhula wa masomo kwa shule za awai, msingi na sekondari kwa mwaka 2026, ambapo kwa mjibu kwa kalenda hiyo shule zitafunguliwa rasmi tarehe 13, Januari 2026.
Baadhi ya wazazi na walezi kutoka kata ya Miyuji jijini Dodoma wamezungumza na taswira ya habari wakieleza jinsi walivyojiandaa kuhakikisha watoto wao wanarudi shuleni kwa wakati, huku wakisisitiza umuhimu wa elimu kwa watoto.
Hata hivyo licha ya dhamira hiyo, wazazi wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika maandalizi hayo ikiwemo ongezeko la gharama za mahitaji ya shule hususani vitambaa vya kushonea sare pamoja na viatu, hali ambayo imeongeza mzigo wa kifedha kwa baadhi ya familia.