Dodoma FM
Dodoma FM
2 January 2026, 3:38 pm

“Ndugu zangu, miti ina faida nyingi tuitikie wito huu. Dhamira ya mheshimiwa rais wetu ni njema sana ndio maana aliwaagiza TFS kuandaa miche kila mwaka na kugawia wananchi bure ili waipande hali itakayohamasisha wengine kupenda mazingira na kupanda miti” alisema Senyamule.
Na Mwandishi Wetu.
Mkoa wa Dodoma umeendelea kutekeleza agizo la serikali la kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kupitia kampeni ya upandaji miti ambapo zoezi hilo limefanyika katika Hospitali ya Jiji la Dodoma iliyopo Nala kwa lengo la kuhamasisha wananchi kupanda miti ya aina zote ikizingatiwa ni msimu wa mvua.
Akizungumza baada ya kushiriki zoezi hilo la upandaji miti, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliwashukuru wadau na wananchi kwa kushiriki katika zoezi hilo, akibainisha kuwa ni muhimu na lenye tija kwa wananchi ambapo mkoa wa Dodoma ulipewa agizo la kuhakikisha unanufaika na rasilimali ya miti.

Alisema kuwa upandaji miti una faida nyingi ikiwemo kutoa kivuli, kuboresha upatikanaji wa hewa safi, kupata matunda pamoja na kusaidia kupambana na ukame uliokithiri kutokana na ukataji miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu uliofanyika hapo nyuma.
Aliongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, serikali inahamasisha wananchi kupanda miti ili kufikia lengo la kuifanya Dodoma kuwa ya kijani, huku akisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kupanda angalau miche mitatu ili kuharakisha urejeshaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa Jiji la Dodoma limejikita kikamilifu katika kutunza mazingira na limeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanahamasishwa kushiriki katika upandaji miti.
Alhaj Shekimweri alieleza kuwa jitihada hizo zinalenga kuikijanisha Dodoma na kuufanya kuwa mji wenye mazingira rafiki kwa afya ya binadamu na ustawi wa vizazi vijavyo. “Jiji la Dodoma linaendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kupanda na kutunza miti, kwa sababu jukumu la kulinda mazingira ni la kila mtu. Tuhakikishe jiji linakuwa la kijani ili hata wageni wanapokuja wafurahie mandhari watakayoyakuta. Mfano huu tulioufanya leo ni kielelezo mojawapo cha kuwahamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi. Tunawahimiza kupanda miti ya kivuli na ya matunda ili faida ziwe nyingi” alisema Alhaj Shekimweri.
Kampeni hiyo katika Hospitali ya Jiji la Dodoma ni muhimu ambapo itakwenda kuhakikisha shule za umma, vituo vya afya na taasisi zinajiunga katika zoezi hilo ili kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi. Kampeni nyingine zilizofanyika ni pamoja na Mti Wangu Birthday yangu, Kijanisha Dodoma na nyinginezo ambazo zimefanikiwa kutoa hamasa ya vitendo na kwa hatua nzuri maeneo mengi yamepandwa miti.