Dodoma FM
Dodoma FM
22 December 2025, 3:33 pm

Wakulima wanaamini kuwa utekelezaji wa haraka wa miradi hiyo utaongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza utegemezi wa misaada ya dharura.
Na Mariam Kasawa.
Wakati Tanzania inatarajia kupata kati ya Dola milioni 5 hadi milioni 20 kupitia mfuko wa upotevu na hasara ,fedha zitakazo saidia jamii zilizoathiriwa na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ,ukiwamo ukame na mafuriko wakulima Mkoani Dodoma wanaiomba serikali kutoa kipaombele kwa sekta ya kilimo kwa kutengeneza miradi ya uvunaji wa maji ya Mvua na utoaji wa Bima kwa wakulima ilikukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi katika sekta hiyo.
Hali ya ukame na mvua zisizotabirika imeendelea kuwa changamoto kubwa kwa wakulima wa Dodoma hali inayosababisha mazao kukauka mashambani na wengine kuvuna kwa hasara, jambo linaloathiri moja kwa moja uzalishaji wa chakula na kipato cha kaya.
Wakulima wanasema miradi ya uvunaji wa maji ya mvua itawasaidia kuendelea na kilimo hata wakati wa mvua chache huku bima ya kilimo itawalinda dhidi ya hasara zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa mujibu wa wataalamu wa tabianchi, maeneo kame kama Dodoma yanahitaji uwekezaji wa haraka katika miundombinu ya kuhifadhi maji, hatua inayotambuliwa kimataifa kuwa msingi wa kulinda usalama wa chakula.
Makubaliano ya kimataifa chini ya umoja wa nchi wanachama wa mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) unazitaka nchi kuingiza miradi ya uvunaji wa maji na bima ya kilimo katika Mipango ya Kitaifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Dokta , Richard Muyungi Mshauri wa Rais katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), anasema Makubaliano ya COP30 yameweka utaratibu wa kufuatilia fedha za tabianchi.
Utekelezaji wa miradi ya uvunaji wa maji ya mvua na bima ya kilimo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kilimo ya mwaka 2013 pamoja na Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.