Dodoma FM

Tanzania yachaguliwa kuwa kituo cha mafunzo ya vijana wa afrika mabadiliko ya tabianchi

17 December 2025, 3:15 pm

Mshauri wa Rais wa katika masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Afrika Dk. Richard Muyungi.Picha na Cop30.

Uamuzi huo unaifanya Tanzania kuwa kituo cha vijana cha Umoja wa Afrika kwa ajili ya kuwajengea uwezo na maarifa katika masuala ya tabianchi.

Na Mwandishi wetu

Tanzania imechaguliwa kuwa kituo cha mafunzo ya vijana wa Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika (AU), hatua inayotajwa kuongeza nafasi ya vijana wa Bara la Afrika kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza kuhusu maazimio ya Mkutano wa COP30 uliofanyika Brazil, Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala ya mazingira na Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika (AGN), Dkt. Richard Muyungi, amesema uamuzi huo unaifanya Tanzania kuwa kituo cha vijana cha Umoja wa Afrika kwa ajili ya kuwajengea uwezo na maarifa katika masuala ya tabianchi.

Dkt. Muyungi amesema kupitia kituo hicho, vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika watapatiwa mafunzo kuhusu uhimilivu wa tabianchi, ubunifu wa suluhisho, uongozi wa kimazingira pamoja na ushiriki wao katika majadiliano ya kimataifa kama COP.

Sauti ya Dkt. Muyungi .

Aidha, ameongeza kwa mwaka huu Tanzania  imeteuliwa kuwa kitovu cha kikanda cha Afrika (African regional hub) katika masuala ya utaalamu wa majanga, kwa lengo la kusaidia uokoaji na usimamizi wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mafuriko, ukame na vimbunga.

Sauti ya Dkt. Muyungi .

kwa mujibu wa Dkt. Muyungi, Hatua hiyo,  ni matokeo ya imani iliyojengwa na jumuiya ya kimataifa juu ya mchango wa Tanzania katika ajenda ya tabianchi barani Afrika, sambamba na msimamo wake katika majadiliano ya COP unaolenga haki ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.