Dodoma FM

Mpwapwa Wananchi Walia, Waomba  Gari la Zimamoto na Uokozi

16 December 2025, 4:17 pm

licha ya Wilaya ya Mpwapwa kuwa miongoni mwa wilaya kongwe nchini, bado haina gari la zimamoto.Picha na Mtandao.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili kulinusuru eneo hilo na majanga ya moto yanayoweza kusababisha hasara kubwa zaidi.

Na Steven Noel.

Wananchi wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma wameiomba Serikali kuwapatia gari la zimamoto na uokoaji ili kujikinga na majanga ya moto yanayoendelea kujitokeza mara kwa mara wilayani humo.

Ombi hilo limetolewa na wananchi wa Mtaa wa Mji Mpya na Ilolo kufuatia tukio la kuungua kwa nyumba ya Bwana Bellen Mbilinyi, mkazi wa Mji Mpya, tukio linalodaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme.

Wananchi hao wamesema kuwa licha ya Wilaya ya Mpwapwa kuwa miongoni mwa wilaya kongwe nchini, bado haina gari la zimamoto, hali inayosababisha changamoto kubwa wakati wa kukabili majanga ya moto, japokuwa kuna askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliopo wilayani hapo.

Mpwapwa ni wilaya yenye taasisi nyingi za Serikali zenye mkusanyiko mkubwa wa watu, zikiwemo shule na vyuo mbalimbali kama Chuo cha Ualimu Mpwapwa, LITA Mpwapwa, Chuo cha Maafisa Afya, Chuo cha Jamii Chisalu, pamoja na shule nyingi za sekondari.

Wananchi wameeleza kuwa hivi karibuni kumekuwepo na matukio kadhaa ya moto yaliyopelekea uharibifu wa mali kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kuzimia moto.

 Wamesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na askari wa zimamoto, wakati mwingine hulazimika kutumia ndoo za mkono kuzima moto, hali inayoongeza hatari na kuchelewesha uokoaji.

Habari kamili.