Dodoma FM
Dodoma FM
15 December 2025, 3:30 pm

Kipindi hiki cha sikukuu, LATRA imeimarisha ukaguzi wa vyombo vya usafiri ili kuhakikisha magari yako katika hali salama, yana bima halali na hayazidishi abiria.
Na Anwary Shaban.
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma wameendelea kushirikiana kwa ukaribu kuhakikisha usalama wa usafirishaji unakuwa bora katika kipindi hiki cha sikukuu.
Akizungumza na Dodoma FM, Afisa Mfawizi wa LATRA Mkoa wa Dodoma, EzekielEmmanuel, amesema kuwa ushirikiano huo unalenga kulinda usalama wa abiria na mali zao kwa kuhakikisha magari yanayotoa huduma za usafiri wa abiria yanazingatia viwango vya ubora vilivyowekwa kisheria.
Ezekiel amesema kuwa katika kipindi hiki cha sikukuu, LATRA imeimarisha ukaguzi wa vyombo vya usafiri ili kuhakikisha magari yako katika hali salama, yana bima halali na hayazidishi abiria, hatua inayosaidia abiria kuepukana na changamoto wakati wa safari.
Aidha, ameeleza kuwa endapo itabainika mhudumu au mmiliki wa chombo cha usafiri amewatoza abiria nauli isiyo halali, hatua kali za kisheria zitachukuliwa mara moja kwa mujibu wa sheria, ili kutokomeza vitendo vya kupandisha nauli kiholela katika kipindi hiki cha sikukuu.
Kwa upande wao, baadhi ya abiria wanaotumia usafiri wa mabasi ya masafa marefu wamesema hali ya usafiri katika kipindi hiki cha sikukuu kwa ujumla ni nzuri, ingawa changamoto hutofautiana kulingana na eneo anapotoka abiria, hali ya barabara pamoja na wingi wa wasafiri.
Sanjari na hayo, mmoja wa madereva wa Kampuni ya Mabasi ya Champion amesema kuwa hali ya usafiri ni shwari, akibainisha kuwa uwepo wa mabasi mengi umesaidia kupunguza msongamano wa abiria na kuondoa adha ya kusubiri usafiri kwa muda mrefu.