Dodoma FM
Dodoma FM
15 December 2025, 12:21 pm

Kwa sasa DUWASA inazalisha lita za maji Milioni 88 kwa siku, huku lengo ni kuzalisha lita za maji Milioni 121 kwa siku pindi miradi mikubwa ya maji ya Nzuguni Awamu ya Pili, Miji 28 Chamwino, Mji wa Serikali Mtumba, UDOM na Nala itakapokamilika.
Na Mariam Kasawa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph amekemea tabia ya baadhi ya wateja kujihusisha na wizi wa maji, wizi wa mita za wateja na baadhi ya wateja kutolipa ankara zao za maji kwa wakati.
Mhandisi Aron ametoa tahadhari hiyo Leo Disemba 15, 2025 Jijini Dodoma wakati wa Mahojiano Maalum ya kipindi kilichorushwa Mubashara cha Baragumu cha Channel ten.
Amesema kuibuka kwa tabia ya uhujumu wa miundombinu ya maji, hasa wizi wa zaidi ya mita 65 za wateja katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dodoma kunarudisha nyuma juhudi za Mamlaka za kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi.
Mhandisi Aron ameweka bayana kuwa kuanzia mwezi Julai, 2025 hadi sasa imewachukulia hatua za kisheria wateja 89 kwa wizi wa maji na wateja 29 wenye madeni ya muda mrefu kwa kutolipa ankara za maji kwa wakati na kuwatoza faini.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Aron amewaomba wateja, wadau na wananchi wote kuwa na imani na DUWASA, kwani ipo kuwahudumia na kwamba inayo mipango ya muda mfupi, kati na mipango ya muda mrefu ya kuwapatia huduma ya maji ya uhakika wakazi wa Dodoma, ambapo utekelezaji wa miradi inayoendelea, hasa ya muda mfupi ya Pembezoni mwa Jijini la Dodoma itasaidia kufikia lengo la kupunguza mgao wa maji.