Dodoma FM
Dodoma FM
11 December 2025, 4:23 pm

Kutopewa kipaumbele na Kupuuzwa kwa sekta ya kilimo katika Mkutano wa COP30 ni kinyume na miongozo ya kimataifa, jambo linaloweza kuathiri juhudi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Na Mwandishi wetu.
Msikilizaji, leo tunakuletea makala ambayo itaangazia Mkutano wa Kimataifa wa Nchi Wanachama wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP30, uliohitimishwa Novemba 22 huko Belém, Brazil, ambapo sekta ya Kilimo haikupewa kipaumbele katika Mkutano huo.
Sekta ya kilimo, inatajwa kuwa ni uti wa mgongo wa nchi za Afrika, lakini katika hali isiyo ya kawaida haikupata kipaumbele cha kujadiliwa inavyostahili katika mkutano huo, jambo ambalo limeibua wasiwasi mkubwa kwa mataifa ya bara hili, ikiwemo Tanzania.
Awali, kilimo na uhakika wa chakula ilikuwa moja ya vipaumbele muhimu katika mkutano huo, ikitengewa siku mbili maalum Novemba 19 na 20, sambamba na mada nyingine za kilimo, mifumo ya chakula, uvuvi, na kilimo cha familia. Hata hivyo, ratiba hiyo haikutoa fursa ya kutosha bali kilimo kiliingizwa tu katika kipengele cha hasara na uharibifu.
Profesa Peter Msofe, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), akizungumza kwa niaba ya mataifa 54 ya Afrika, alisisitiza umuhimu wa kilimo kama chanzo kikuu cha chakula, ajira, na ustawi wa wananchi.
Aliweka wazi kwamba, kupuuzwa kwa kilimo ni tishio kwa mustakabali wa maendeleo ya Afrika, hasa katika zama hizi ambapo mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiwango kikubwa mavuno na upatikanaji wa chakula.
Katika COP29, iliyofanyika Novemba 11–22, 2024 huko Baku, Azerbaijan, kulikuwa na Siku Maalum ya Chakula, Kilimo na Maji, ambapo kilimo na mifumo ya chakula vilijadiliwa kwa kina. Hii iliasisi Mkakati wa Tabianchi wa Harmoniya Baku kwa Wakulima, kwa ushirikiano na Shirika la chakula na kilimo la umoja wa mataifa (FAO), kusaidia wakulima wadogo na jamii vijijini.
Profesa Eliyakimu Zahabu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) anaonya kwamba kupuuzwa kwa kilimo katika COP30 kunaweza kuathiri uwezo wa Afrika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Umoja wa nchi wanachama wa mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC)unasiitiza kilimo na mifumo ya chakula lazima iwe mstari wa mbele katika majadiliano ya kimataifa, ikijumuisha mbegu himilivu, bima, na mifumo ya maji.
Makubaliano ya Paris Agreement 2015 yanatambua kilimo kama sekta ya kipaumbele ikihimiza ajira, usalama wa chakula, na ustahimilivu wa wakulima katika majadiliano ya kitaifa.
Jakson Machila, mkulima kutoka Chamwino, Mkoani Dodoma, anasema kutokupewa kipaumbele sekta ya kilimo katika mkutano huo kunasababisha ukosefu wa ufadhili wa teknolojia na tafiti muhimu.
Pamoja na kwamba kilimo hakijapewa kipaombele katika mkutano wa COP30nchi za Afrika ikiwemo Tanzania bado kunaumuhimu wa kukipa kipaombele kilimo ilikusaidia wakulima wadogo na jamii za vijiji ambazo zinategemea kilimo kama chanzo kikuu cha mapato.