Dodoma FM
Dodoma FM
27 November 2025, 3:20 pm

Wadau wa maendeleo wanaotekeleza afua za usalama wa watoto mtandaoni wameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya aina zote za ukatili, hususan ukatili wa mtandaoni.
Na Mariam Matundu.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wanapotumia mitandao hasa kipindi cha likizo.
Akizungumza na watoto wa Shule ya Msingi Martin Luther jijini Dodoma, Novemba 26, 2025, Dkt.
Gwajima amesema pamoja na teknolojia kuongeza fursa, imeibua pia hatari mbalimbali kwa watoto.
Amesema utafiti wa mwaka 2022 umeonesha kuwa watoto wameendelea kukumbana na ukatili mtandaoni, ikiwemo kushawishiwa kutuma picha zisizofaa na kukutana na wahalifu wanaojificha kwenye majukwaa ya mtandaoni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Sebastian Kitiku, amewashauri watoto wote nchini kutumia vifaa vya kielektroniki kwa umakini na ufasaha wakiwa nyumbani, hususan kipindi cha likizo ndefu ili kuepusha hatari zinazoweza kuhatarisha usalama wao.