Dodoma FM
Dodoma FM
17 November 2025, 3:50 pm

Hata hivyo, madereva hao wamebainisha changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo kutoaminika na baadhi ya watu kutokana na jinsia yao, hali ambayo wamesema inapaswa kubadilika ili kutoa nafasi sawa kwa wote.
Na Farashuu Abdallah.
Wanawake nchini wametakiwa kuondoa hofu ya kujifunza fani ya udereva, kwani ni kazi kama zilivyo kazi nyingine na yenye heshima katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Madereva Wanawake Tanzania, Bi. Naetwe Herini Ihema, wakati akizungumza na kituo cha Dodoma FM.
Amesema ni wakati muafaka kwa wanawake kujiunga na mafunzo ya udereva wa magari makubwa, roli, meli na magari madogo, ili kuongeza nafasi zao katika soko la ajira.
Bi. Ihema amewahimiza madereva wanawake kujiunga na Chama cha Madereva Wanawake Tanzania, ambacho kwa sasa kinawahudumia zaidi ya wanachama 1,200 nchini, ili kupata mafunzo yatakayowaongezea ujuzi na kuaminika zaidi katika jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva wanawake wamesema chama hicho kimekuwa msaada mkubwa kwao, kwani kimewajengea uaminifu na uwezo wa kufanya kazi kwa weledi. Wameiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono na kuwapa nafasi katika soko la ajira, wakisisitiza kuwa wanawake ni madereva makini na wa kuaminika.