Dodoma FM
Dodoma FM
13 November 2025, 4:27 pm

Wananchi hao wameomba kuwekwa utaratibu wa uhakika wa upatikanaji wa maji ili kupunguza usumbufu wanaoupata.
Na Farashuu Abdallah.
Wakazi wa Mtaa wa Mathias, Kata ya Miyuji jijini Dodoma wameiomba serikali kutatua changamoto ya ukosefu wa maji ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Wakizungumza na Dodoma Fm wananchi wamesema upatikanaji wa maji umekuwa wa kusuasu, jambo linaloathiri shughuli zao za kila siku za nyumbani, huku wakiomba kuwekwa utaratibu wa uhakika wa upatikanaji wa maji ili kupunguza usumbufu wanaoupata.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mathias Bi. Doreen Deogratius, amesema amepokea tatizo hilo na tayari ameanza mikakati ya kulipatia suluhu ikiwemo kuchimba visima vya maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DUWASA).
Aidha, Bi. Doreen amewataka wakazi wa mtaa huo kuwa na uvumilivu wakati juhudi za kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi zikiendelea kufanyika.