Dodoma FM
Dodoma FM
13 November 2025, 4:09 pm

Zoezi hilo lilianza Novemba 12 na linatarajiwa kukamilika Novemba 14, 2025, huku wataalamu wa afya wakiendelea kutoa elimu kuhusu kinga, umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili, na matumizi sahihi ya vyakula vinavyosaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza.
Na; Lilian Leopold.
Wananchi jijini Dodoma wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza,linaloambatana na utoaji wa elimu ya afya kuhusu magonjwa mbalimbali.
Wito huo umetolewa na Dkt. Bryceson Kiwelu, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Mifupa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Novemba 12, katika Maadhimisho ya Wiki ya Upimaji wa Magonjwa yasiyoambukiza yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma.

Baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kufanyiwa vipimo hivyo wameshukuru wadau wa afya kwa kuandaa zoezi hilo, wakisema limewasaidia kujua hali zao za kiafya na kuchukua tahadhari mapema.