Dodoma FM
Dodoma FM
10 November 2025, 3:36 pm

Kwa mujibu wa tafiti zilizotajwa, mitandao ya kijamii inaonekana kuwa na athari kubwa zaidi kwa vijana walioko katika kipindi cha kubalehe, ikilinganishwa na muziki, filamu, au hata marafiki wa karibu.
Na Farashuu Abdallah.
Jamii imetakiwa kuwekeza kwa dhati katika malezi ya vijana ili kuwa chachu ya kuleta mtindo bora wa maisha na kuzuia mmomonyoko wa maadili unaoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Wito huo umetolewa na Mtaalamu wa Saikolojia ya Kijamii, Mtahu Mtahu, wakati akizungumza na kituo cha redio cha Dodoma FM, ambapo amesema ni muhimu kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwekeza katika malezi bora ya vijana kwa kuwaandaa katika misingi ya maadili, utamaduni, na tabia njema.
Mtahu amesema malezi bora ndiyo msingi wa tabia njema, na kwamba jamii isipochukua hatua sasa, kizazi kijacho kitaathirika kwa kiasi kikubwa.
Aidha, amewashauri vijana kuwa makini na mambo yanayoathiri mitindo yao ya maisha, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, kuangalia filamu zisizo na maadili, pamoja na kushirikiana na marafiki wasio na mwelekeo chanya.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wamewahimiza wazazi na walezi kuwa na utamaduni wa kukaa na vijana wao, kuwapa mwelekeo sahihi wa maisha na kuwajengea msingi wa maadili mema.