Dodoma FM

Sababu za kisaikolojia zatajwa tatizo la afya ya akili

22 October 2025, 4:18 pm

Magonjwa ya akili yanaweza kutokea kutokana na sababu za kibaiolojia, ikiwa ni pamoja na kurithi kutoka kwa wanafamilia.Picha na mtotonews.com.

Jamii inapaswa kuondoa unyanyapaa dhidi ya watu wanaopitia changamoto za afya ya akili na badala yake, kuwasaidia kwa upendo na msaada wa kitaalamu.

Na Peter Nnunduma.
Sababu za kisaikolojia kama vile msongo wa mawazo, kupoteza mtu wa karibu na ajali vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu za ugonjwa wa afya ya akili.

Hayo yamebainishwa na Mwanasaikolojia Maurida Hassan katika mahojiano aliyofanya na Dodoma FM ambapo amesema kuwa afya ya akili ni hai ya mtu kuwa na uwezo wa kufikiri vizuri, kuhisi kwa usahihi, na kuwa na mahusiano mazuri na wengine.

Ameongeza kuwa magonjwa ya akili yanaweza kutokea kutokana na sababu za kibaiolojia, ikiwa ni pamoja na kurithi kutoka kwa wanafamilia, mabadiliko ya kemikali katika ubongo, au matatizo ya muda mrefu ya kiafya kama kisukari au saratani.

Sauti ya Maurida Hassan.

Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya matatizo ya akili yanahitaji ushirikiano wa wadau wote, wakiwemo wazazi, walimu, waajiri, viongozi wa dini na serikali kwa ujumla lakini pia, kushiriki mazoezi ya mwili, kula lishe bora, kulala vizuri na kujiepusha na matumizi ya vilevi kama sehemu ya kujikinga na matatizo ya afya ya akili.

Sauti ya Maurida Hassan.

Kwa mujibu wa takwimu za Septemba 2025 za Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa, W-H-O zinazohusina na masula ya Afya ya akili zinaeleza kuwa zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na changamoto za afya ya akili kama vile msongo wa mawazo na mfadhaiko. Hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa wataalam wa afya.