Dodoma FM

Serikali yazindua mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima

21 October 2025, 3:35 pm

Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Zuhura Yunus katika mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima na wazalishaji wadogo. Picha na Selemani Kodima.

Mafunzo haya yanatolewa kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), yakilenga kuwajengea wakulima uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa mazao na kupata masoko ya uhakika.

Na Selemani Kodima.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imezindua rasmi mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wakulima na wazalishaji wadogo katika sekta ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea viwanda na nguvukazi yenye maarifa na ujuzi.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Zuhura Yunus amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, wakulima wapatao 1,000 kutoka mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Mbeya watanufaika na mafunzo ya vitendo yanayolenga kuboresha uzalishaji, kuongeza ubora wa bidhaa na kukuza kipato cha mtu binafsi pamoja na pato la taifa.

Naibu Katibu Mkuu amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wakulima wadogo wanapanda ngazi hadi kufikia kiwango cha kati na hatimaye cha juu, sambamba na azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutomwacha nyuma mdau yeyote katika safari ya maendeleo.

Aidha, ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo kutumia vyema fursa waliyoipata na kuwa mabalozi wa mabadiliko katika jamii zao. Viongozi wa TARI, Wakuu wa Mikoa, Halmashauri na wadau wengine wametajwa kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya programu hii.