Dodoma FM
Dodoma FM
14 October 2025, 1:46 pm

Watoto wenye ulemavu wa utindio wa ubongo wanahitaji msaada wa kitabibu, lishe, na mazoezi, huku wazazi wakipokea mwongozo kutoka serikalini na taasisi za kiraia.
Na Anwary Shaban.
Watoto wenye ulemavu wa utindio wa ubongo wanakabiliwa na changamoto za kupata huduma za kitabibu, lishe maalum, na mazoezi ya mwili.
Bi. Shemza Kayuga, Mkurugenzi wa Taasisi ya Joy of Hope, amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kupitia hafla ya Maadhimisho ya Siku ya watoto wenye mtindio wa ubongo iliyoandaliwa na taasisi hiyo kwa lengo la kutoa msaada wa huduma za kitabibu, lishe maalum na mazoezi ya mwili yanayohitajika kuwaweka watoto hao katika hali bora.
Amebainisha changamoto zinazowakabili watoto hao ni pamoja na ukosefu wa huduma za kitabibu, lishe maalum, na mazoezi ya mwili.
Aidha, Bi. Kayuga ameongeza kuwa taasisi yake itaendelea kuwa bega kwa bega na familia hizo, ikiwemo kutoa mwongozo wa kisaikolojia, lishe, na huduma nyingine muhimu kwa watoto wenye ulemavu wa utindio wa ubongo.

Nao baadhi ya wazazi wameitaka jamii kutowaficha watoto wenye ulemavu wa utindio wa ubongo bali kuwapa nafasi sawa ya kupata matibabu na elimu kama watoto wengine.
Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Katibu Tawala, Bi. Sakina Mbugi, amesema serikali itaendelea kushirikiana na jamii na taasisi zinazohusika ili kuhakikisha watoto hawa wanapata lishe bora, huduma za afya, na elimu stahiki.
Siku ya watoto wenye ulemavu wa utindio wa ubongo huadhimishwa tarehe 11 Oktoba kila mwaka na mwaka huu imebaba kauli mbiu inayosema “Ujumuishi, Tumaini na Heshima kwa Watoto Wenye Mtindio wa Ubongo”.