Dodoma FM
Dodoma FM
14 October 2025, 1:02 pm

Kutokana na changamoto hiyo wananchi waiomba serikali kuongeza nguvu ya umeme ili kukidhi mahitaji ya jamii.
Na Victor Chigwada.
Wakazi wa Kitongoji cha Kawawa, Kijiji cha Chanhumba, wameiomba serikali kuongeza nguvu ya upatikanaji wa nishati ya umeme katika eneo hilo, wakieleza kuwa licha ya umeme kuwafikia, haujitoshelezi kuhudumia jamii nzima.
Wamesema umeme huo umekuwa ukikatika mara kwa mara kutokana na kuzidiwa nguvu pindi mashine au vifaa vya umeme vinapotumika, hasa katika zahanati na shughuli nyingine za kijamii.
Wakazi hao wameeleza kuwa kwa sasa baadhi yao wanatumia nishati ya jua (solar) kwa matumizi madogo madogo, lakini wamebainisha kuwa umeme wa gridi ni muhimu zaidi katika kuendesha viwanda vidogo vitakavyosaidia kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa kijiji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chanhumba, Ndg. Amosi Lusiji, amesema mashine ya kufua umeme iliyopo kwa sasa haiwezi kukidhi mahitaji ya wananchi wote kutokana na matumizi makubwa yanayoshirikishwa kati ya kaya, zahanati, na mashine mbalimbali za uzalishaji.
Amesema changamoto hiyo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo za wakazi wa Kawawa na ameiomba Serikali kuongeza nguvu au kuleta chanzo kipya cha nishati ili kuimarisha huduma hiyo muhimu.