Dodoma FM

Wanasiasa wahimizwa kufanya kampeni kwa amani

13 October 2025, 11:51 am

Viongozi kisiasa watakiwa kutambua umuhimu wa kulinda amani ya nchi kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. Picha na Mtandao.

Rai hiyo imetolewa na Askofu Evance Chande alipokuwa akihubiri kwenye ibada iliyofanyika kanisani hapo lililopo Ipagala Mkoani Dodoma.

Na Selemani Kodima.

Askofu Mkuu wa Kanisa Karimel Assembelis of God Tanzania Dkt. Evance Chande amewataka wanaogombea nafasi ya Urais,Ubunge na Udiwani kufanya kampeini zao kwa ustaharabu na zisizo chochea uvunjifu wa amani na kuwagombanisha watanzania .

Katika mahubiri yake Askofu Dk. Evance amesema kuwa pamoja na mambo mengine waliyonayo watanzania na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa wanatakiwa kutambua umuhimu wa kulinda amani ya nchi kwenye kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa kuwachagua Rais,Wabunge na Madiwani.

Katika hatua nyingine Askofu huyo amewaomba watanzania kuendelea kumwomba Mungu kwenye kipindi hiki cha kufanya uchaguzi, ili kuweza kufikia malengo ya kuwapata viongozi kwa njia ya amani na utulivu.

Amesema kuwa viongozi wa dini hawaegamii chama chochote cha siasa lakini ni wajibu wa kanisa kuwaomba watanzania kufanya maombi ili Mungu ahusike katika kupatikana kiongozi bora.

Amesema kuwa kama kanisa halina ushabiki wa chama chochote lakini linao wajibu wa kuombea wagombea na taifa ili Mungu apitishe viongozi waaminifu na wenye hofu ya Mungu na wasiopenda chokochoko ambazo zinaweza kusababisha kutoweka kwa amani ya nchi.