Dodoma FM
Dodoma FM
13 October 2025, 10:45 am

Baadhi ya wananchi wamegundulika kuwa na tatizo la mtoto wa jicho, jambo lililosababisha changamoto za kuona kwa baadhi yao. Picha na Mtandao.
Kupitia kambi ya huduma za macho, wagonjwa hao wamepatiwa matibabu ikiwemo upasuaji mdogo, hatua iliyowawezesha kurejesha uwezo wao wa kuona na kuboresha ubora wa maisha yao.
Na Mariam Kasawa.
Imeelezwa kuwa zaidi ya watu 100 walijitokeza kupima afya ya macho, ambapo 10 kati yao wamegundulika kuwa na matatizo ya macho, hususani tatizo la mtoto wa jicho.
Hospitali ya Benjamin Mkapa imeendesha kambi maalum ya huduma za macho katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino, ambapo wananchi mbalimbali wamepatiwa huduma za uchunguzi na matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Amon Mwakakonyole, amesema kupitia kambi hiyo wamefanikiwa kuwasaidia wagonjwa waliokuwa wamepoteza uwezo wa kuona, ambao sasa wanaendelea kuona vizuri.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Macho Wilaya ya Chamwino, Bw. Yona Ndaiga, amesema eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto kubwa ya matatizo ya macho, ikiwemo tatizo la mtoto wa jicho.
Ameishukuru Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kujitolea kutoa huduma hizo muhimu kwa wananchi ambao kwa muda mrefu hawakuwa wamefikiwa na huduma hizo.
Baadhi ya wananchi waliopatiwa huduma, wakiwemo waliokuwa na matatizo yaliyohitaji upasuaji, wameeleza kufurahishwa na huduma walizopata na kuwashukuru wataalamu kwa jitihada zao.
Sauti za wananchi.