Dodoma FM
Dodoma FM
10 October 2025, 3:16 pm

Kupitia siku hii, jamii inatakiwa kutambua umuhimu wa mayai, kwani kupitia ulaji wa mayai, familia zinaweza kupunguza utapiamlo na kuimarisha afya za watoto.
Na Anwary Shaban.
Siku hii, inayoadhimishwa kila mwaka mwezi Oktoba, inalenga kuongeza uelewa kuhusu nafasi ya yai katika kuboresha afya ya binadamu kutokana na protini, vitamini, na madini muhimu yaliyomo ndani yake.
Akifanya mahojiano na Taswira ya Habari Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Beatrice Moshi amesema yai husaidia ukuaji wa watoto, kuimarisha nguvu za watu wazima, na kulinda afya ya ubongo kwa rika zote.
Aidha, Bi. Moshi ameongeza kuwa mayai yanapendekezwa zaidi kwa makundi maalum kama watoto wa umri wa miaka 6 na kuendelea, wanawake wajawazito, watu wenye udhaifu wa mwili, wazee, na wale walioko katika matibabu ya kurejesha afya.

Kwa upande wao, wafanyabiashara wa mayai wamesema wanazingatia ubora wa bidhaa kuanzia kwa wauzaji wa jumla hadi kwa watumiaji wa mwisho.
Nao baadhi ya wananchi wamesema kuwa yai limekuwa sehemu ya mlo wa kila siku. Wameeleza faida zake ikiwa ni pamoja na kumjenga mtoto kiakili na kuongeza protini mwilini.
Siku ya Yai Duniani ilianzishwa rasmi mwaka 1996 na Shirika la Kimataifa la Yai (International Egg Commission), na imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha jamii kuhusu faida za yai katika maisha ya binadamu.