Dodoma FM

Jamii yaaswa kuacha kuwabeza makondakta wanawake

6 October 2025, 5:07 pm

Kazi ya ukondakta ni kazi kama kazi nyingine, hivyo wanawake wana nafasi sawa ya kuifanya bila kubaguliwa. Picha na Blog.

Amesema wanawake hao wamekuwa wakijituma kama watu wengine katika kutafuta kipato, ili kuhakikisha familia zao zinapata mahitaji ya msingi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Na Anwary Shaban.

Jamii imeaswa kuacha mitazamo hasi dhidi ya wanawake wanaofanya kazi za ukondakta, kwa kuwa kazi hizo si za wanaume pekee bali ni chanzo halali cha kipato kwa wanawake wanaowajibika katika familia zao.

Fatma Kibasa kutoka Taasisi ya Action For Community Care, amesema hayo wakati akizungumza na Taswira ya Habari ya Dodoma FM, ambapo amesisitiza kuwa wanawake wanaofanya kazi za ukondakta wanapaswa kuungwa mkono badala ya kubezwa.

Amesema wanawake hao wamekuwa wakijituma kama watu wengine katika kutafuta kipato, ili kuhakikisha familia zao zinapata mahitaji ya msingi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.

Sauti ya Fatma Kibasa.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dodoma, hususan wanaotumia usafiri wa daladala, wamesema ni jambo la kupongezwa kuona wanawake wakijitokeza kufanya kazi halali bila kujali mtazamo wa kijamii, kwani kila mtu ana haki ya kufanya kazi yoyote inayompatia kipato.

Sauti za abiria.

Kwa upande wake, dereva wa daladala anayefanya kazi na kondakta mwanamke amesema wanawake hao wanafanya kazi kwa bidii na uaminifu, japokuwa changamoto kubwa wanazokutana nazo ni majukumu ya kifamilia ambayo mara nyingi huathiri muda wao wa kazi.

Sauti ya dereva.

Naye Lightnes Tindwa, mmoja wa wanawake wanaofanya kazi za ukondakta jijini Dodoma, amesema alianza kazi hiyo kwa lengo la kusaidia familia yake, na sasa anaiona kama kazi ya kawaida licha ya mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu.

Sauti ya Lightnes Tindwa.