Dodoma FM
Dodoma FM
6 October 2025, 11:11 am

Picha ni Mganga Mkuu jiji la Dodoma Dkt. Pima Sebastian na wadau wakifungua jengo la mama na mtoto zahanati ya Chamwino. Picha na Lilian Leopold.
Mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018 na kukamilika mwezi Septemba 2025, umekuwa miongoni mwa juhudi za kuimarisha miundombinu ya afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Na Lilian Leopold.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kushirikiana na Shirika la World Vision kupitia mradi wa Ahadi imekamilisha ukarabati wa jengo la mama na mtoto katika Zahanati ya Chamwino, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto kwa wananchi wa eneo hilo.
Mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018 na kukamilika mwezi Septemba 2025, umekuwa miongoni mwa juhudi za kuimarisha miundombinu ya afya na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma za uzazi salama na huduma rafiki kwa vijana katika zahanati hiyo, Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Pima Sebastian, amewataka wahudumu wa afya kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji huduma kwa wananchi, ikiwemo kutunza siri za wagonjwa na kutoa huduma kwa upendo na utu.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Chamwino, Dkt. Alano Stanley, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo , amesema kuwa gharama za awali za jengo hilo zilikuwa shilingi milioni 85, huku ukarabati na maboresho mapya yakigharimu shilingi milioni 18, na kufanya jumla ya matumizi kufikia shilingi milioni 103.
Amesema ukarabati huo umehusisha ujenzi wa vyumba vya kujifungulia, vyoo bora, chumba cha upasuaji mdogo, pamoja na maboresho ya mfumo wa maji na umeme ili kurahisisha utoaji wa huduma bora za afya kwa mama na mtoto.