Dodoma FM
Dodoma FM
1 October 2025, 4:00 pm

Pichani ni baadhi ya wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe kata ya Matumbulu. Picha na Lilian Leopold.
Elimu hii inalenga kupunguza tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri wa miaka mitano na kushuka chini.
Na Lilian Leopold.
Wananchi wa Mtaa wa Kaunda, Kata ya Matumbulu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wamepatiwa elimu muhimu kuhusu lishe bora na malezi ya watoto, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe.
Happiness Benard Chibinda, Mtendaji wa Mtaa wa Kaunda, amesema kuwa maadhimisho hayo yamewapa wazazi na walezi uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora katika ukuaji wa watoto. Amesisitiza kuwa malezi bora yanachangia katika kupunguza udumavu na kuboresha afya ya watoto.
Aidha ametoa wito kwa wanaume kushiriki katika suala la lishe kwani jukumu hilo situ la mama bali ni la wazazi wote na jamii nzima.

Kwa upande wake Mtaalam wa afya ngazi ya jamii William Daud amewasisitiza wazazi na walezi kuzingatia suala la unyonyeshaji kwa watoto ikiwemo kunyonyesha kwa wakati na kuzingatia makundi ya vyakula ili kujenga kinga ya mwili ya mtoto na kupunguza hatari ya magonjwa.
Maadhimisho haya ni sehemu ya juhudi za serikali ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora na malezi ya watoto, ili kuhakikisha watoto wanakua wakiwa na afya njema na kuwa na mchango chanya katika maendeleo ya taifa.