Dodoma FM
Dodoma FM
29 September 2025, 3:10 pm

Kongamano hilo limewakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani Dodoma na maeneo jirani, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu namna ya kuripoti habari za uchaguzi kwa ufanisi, pamoja na kuongeza ulinzi na usalama wa waandishi hao katika kipindi cha kampeni na uchaguzi mkuu.
Na Anwary Shaban.
Waandishi wa habari nchini wameaswa kutoa taarifa sahihi na kuzingatia usawa katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025, ili kuepuka upotoshaji wa taarifa na kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde, wakati akifungua kongamano maalum la waandishi wa habari lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (DPC), lililofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mhe. Mavunde amewataka waandishi wa habari kuwa na weledi wa kutosha, kuzingatia maadili ya taaluma yao na kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi, zenye mizania, bila kuegemea upande wowote katika kipindi cha uchaguzi.

Kwa mujibu wa Mavunde, vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha amani, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi, na kwamba kwa kufanya hivyo kwa weledi, vinaweza kusaidia kuimarisha misingi ya demokrasia nchini.