Dodoma FM

Uzembe kisheria unavyoharibu mazingira Dodoma sehemu ya 2

29 September 2025, 2:13 pm

Picha ni eneo la wazi katika mtaa wa changanyikeni ambalo wananchi wameligeuza kuwa dampo.Picha na Noah Patrick.

Utupaji wa taka ovyo unatajwa kuharibu mazingira kwa kiasi kikubwa kwa kusababisha taka nyingi kusambaa ovyo.

Na Mariam Kasawa.

Msikilizaji, leo tunazungumzia Kutotekelezwa kwa sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 sura 20 kufungu cha 114-116 kumesababisha kulundikana kwa taka za majumbani katika mitaa ya Chanagnyikeni, Kibaoni na St Gemma katika kata ya Miyuji Jijini Dodoma.

Kutotekelezwa kwa sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 sura 20 kufungu cha 114-116 kumesababisha kulundikana kwa taka za majumbani katika mitaa ya Chanagnyikeni, Kibaoni na St Gemma katika kata ya Miyuji Jijini Dodoma.

Jiji ya Dodoma inakisiwa kuzalisha tani 350 za taka ngumu kwa siku ambapo kata za nje ya mji uzalishaji tani 114 na Kata za mjini uzalisha ni tani 236. Aidha wastani wa tani 150 tu ndiyo zinaondoshwa mjini kwa siku sawa na asilimia 66%, hali hiyo imekuwa ikichangiwa na uhaba mkubwa wa vifaa hasa Skip bucket kwani kwa sasa zipo 61 kati ya 187 zinazohitajika kwa sasa kwa mujibu wa mwongozo.

Mfuko wa taka ukiwa umetelekezwa katika eneo la wazi mitaa ya kibaoni.Picha na Noah Patrick.

Uzoaji wa taka katika maeneo mbalimbali ya mji, vikundi vya kijamii vimekuwa vinatoa huduma ya kuzoa taka katika ngazi ya kaya, na maeneo mbalimbali ya biashara na kupeleka katika vituo vya kupokelea taka (collection point) ambapo kuna makasha ya kupokelea taka (Skip buckets). Halmashauri inasafirisha taka mpaka kwenye dampo la kisasa lililoko eneo la Chidaya Kata ya Matumbulu.

Dampo la Kisasa la Chidaya lina Ukubwa wa Hekari 48 ambapo eneo linalotumika kwa sasa lina Ukubwa wa Hekari 10. Dampo hili lina uwezo wa kutumika kwa muda wa miaka 18 hadi 20.

Dampo hili linapokea taka kila siku kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12 jioni. Taka hupimwa katika mizani iliyopo katika geti la kuingilia dampo ili kujua uzito wake kwa kila gari inayoleta taka Dampo na kutunza takwimu.

Wastani wa tani 120 -150 za taka ngumu hutupwa katika Dampo kila siku kutoka katika vyanzo mbalimbali vya uzalishaji taka.

Kwa mujibu wa malalamiko ya wananchi wa mitaa hii wanadai kuwa licha ya kukosa huduma ya gari la kuzoa taka kama ilivyo kwa maeneo mengi hapa jijini ambapo gari hilo hupita mara moja au mbili kwa wiki kukusanya taka pia wamekuwa wakikumbana na kadhia ya baadhi ya watu kuwalipa maafisa usafirishaji almaarufu kama bodaboda  pesa na kuwapa mizigo ya taka ambayo huenda kuitelekeza katika maeneo ya wazi katika kata hiyo ikiwemo kando ya barabara.