Dodoma FM

Tume ya utumishi wa umma kutoa maamuzi ya rufaa 108 jijini Dodoma

26 September 2025, 3:28 pm

Picha ni Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso Akizungumza kuhusu mkutano huo.Picha na Seleman Kodima.

Miongoni mwa sababu zinazojitokeza mara kwa mara katika rufaa hizo ni pamoja na Kukiuka maadili ya utumishi wa umma,Kughushi vyeti au kutoa taarifa za uongo,Uzembe kazini,Wizi wa mali za umma

Na Seleman Kodima.
Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kutoa maamuzi ya rufaa na malalamiko yaliyowasilishwa na watumishi wa umma waliokosa kuridhika na maamuzi ya Mamlaka za Ajira, Waajiri na Mamlaka za Nidhamu.
Mkutano huo muhimu unatarajiwa kufanyika jijini Dodoma kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 17 mwaka huu.
Akizungumza kuhusu mkutano huo, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso, amesema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 12(1)(d) na Kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298, marejeo ya mwaka 2023, Tume ina wajibu wa kupokea na kusikiliza rufaa kutoka kwa watumishi wa umma ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya waajiri wao.

Sauti ya Bw. John Mbisso.

Katika mkutano huo, Tume inatarajia kupitia jumla ya rufaa na malalamiko 108, ingawa idadi hiyo inaweza kuongezeka kutokana na mwendelezo wa utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Aidha, Bw. Mbisso ameongeza kuwa mkutano huo pia utatumika kama jukwaa la kupitia taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya tatu na robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa fedha 2023/2024, Tume ya Utumishi wa Umma ilipokea na kushughulikia jumla ya rufaa na malalamiko 1,015 kutoka kwa watumishi wa umma waliokuwa hawajaridhika na maamuzi ya waajiri au mamlaka za nidhamu.

Sauti ya Bw. John Mbisso.

Tume ya Utumishi wa Umma inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha haki, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma nchini.