Dodoma FM
Dodoma FM
25 September 2025, 4:01 pm

Upanuzi wa barabara unafanyika kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za dharura pindi majanga yatakapojitokeza.
Na Lilian Leopold.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Septemba 24, 2025 limeendelea na zoezi la kupanua barabara ndani ya masoko ambapo limefanyika katika soko la Sabasaba Jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, Afisa wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Dodoma Mjini, Inspekta Deogratius Inano amesema matukio mbalimbali ya majanga yaliyotokea nchini yamekuwa fundisho kwao, na kwamba wamejipanga kuhakikisha hali kama hizo zinakabiliwa kwa haraka.
Baadhi ya wafanyabiashara waliokuwepo wamesema hatua hiyo ni kwa manufaa yao, hivyo hakuna sababu ya kulalamikia uharibifu wa baadhi ya miundombinu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Sabasaba, Kombo Kombo, amesema soko hilo lina zaidi ya wafanyabiashara elfu 14 wanaolitegemea kuendeshea maisha yao, na kwamba zoezi la kupanua njia ni sehemu ya kuhakikisha usalama wao unazingatiwa.