Dodoma FM
Dodoma FM
25 September 2025, 1:58 pm

Wasichana walio katika hatari kubwa ya kupata mimba wapatiwe motisha ili kuwasaidia kumaliza shule kama vile malipo ya kifedha au programu za masomo.
Na Mariam Kasawa.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO limetoa mwongozo mpya wa kimataifa unaolenga kuzuia mimba za utotoni na kuboresha afya za wasichana, likiwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto hii inayowakumba mamilioni ya wasichana duniani.
Mwongozo huu mpya wa WHO unasisitiza umuhimu wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana, upatikanaji wa huduma rafiki kwa vijana, na usaidizi kwa wasichana waliopata mimba au walioolewa wakiwa watoto. Pia, unalenga kushughulikia vikwazo vya kijamii na kisheria vinavyowazuia wasichana kupata huduma za afya ya uzazi.
Takriban wasichana milioni 16 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19, na milioni 2 walio chini ya umri wa miaka 15, hujifungua kila mwaka.
Asilimia 95 ya mimba hizi hutokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, hususan miongoni mwa jamii maskini, zisizo na elimu na za vijijini.
Bara la Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara lina viwango vya juu zaidi vya mimba za utotoni duniani. Hali hii inachangiwa na ndoa za utotoni, ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, na huduma duni za afya.
Hali ni vivyo hivyo, Amerika ya Kusini na Karibiani ambazo nazo zinaendelea kuwa na viwango vya juu vya mimba za utotoni, licha ya maendeleo ya kiuchumi.