Dodoma FM

Senyamule apokea vitendea kazi wahudumu wa afya ngazi ya jamii

5 September 2025, 5:19 pm

Picha ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule akikagua vifaa hivyo .Picha na Mkoa wa Dodoma.

Miradi inawezesha kuwaibua na kuwaunganisha watoto na vijana kwenye matibabu, kuwasaidia kubaki katika huduma na matibabu na kuishi maisha yenye afya.

Na Yussuph Hassan.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule amepokea na kukabidhi vifaa vya michezo, vya kujifunzia pamoja na vitendea kazi vya watoa huduma za afya ngazi ya Jamii ili viweze kuwafikia walengwa waliopo katika baadhi ya Halmashauri za Mkoa huu.

Akizungumza na baadhi ya wadau na watoa huduma ngazi ya Jamii amesema Mkoa unashirikiana na Shirika la Action for Community Care (ACC) katika kutekeleza miradi ya Imarisha Afya na ‘ViiV Pediatric Breakthrough Partnership’ ambayo inalenga kusaidia watoto na vijana wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wenye umri wa miaka 0 -19.

Sauti ya Mhe.Rosemary Senyamule.

Miradi hiyo ililenga pia kuwatambua na kutoa mafunzo kwa Wakunga wa Jadi kwa lengo la kuwaelekeza kuhusu umuhimu wa kuwaelimisha wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa usalama wao na watoto watakaozaliwa.

Kwa upande wake Meneja wa Miradi Bi.Melina Mgongo amesema ACC ni shirika lisilo la Kiserikali na linatekeleza shughuli zake katika Halmashauri 04 za Mkoa wa Dodoma Ikiwemo Kongwa,Chamwino, Mpwapwa na Dodoma Mjini.

Maeneo ya utekelezaji wa miradi ya ACC ni elimu,afya na lishe, ulinzi na usalama,Kuboresha na kuimarisha kipato katika ngazi ya familia na mazingira.

Sauti ya Bi.Melina Mgongo.