Dodoma FM

Fidia bil. 2.6 kulipwa Septemba waliopisha mradi wa umeme Kagera

26 August 2025, 2:59 pm

Picha ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika hafla ya utiaji saini mikataba ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme .Picha na Seleman Kodima.

Dkt Biteko amesema baada ya miaka michache, Mkoa wa Kagera hautakuwa na changamoto ya umeme.

Na Seleman Kodima.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ameagiza wananchi waliopisha mradi wa Umeme Kagera walipwe fidia haraka.

Agizo hilo amelitoa leo jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini mikataba ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kwa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benako hadi Kyaka, pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Beneko chenye msongo wa kilovoti 220/33.

Amesema kuwa Serikali imeamua kwa dhati kazi hiyo kufanyika Kagera na baada ya muda itakuwa chanzo kikubwa cha umeme.

Picha ni picha ya pamoja kati ya Naibu waziri mkuu na wa waziri wa nishati na wageni wengine katika hafla hiyo.Picha na Seleman Kodima.

Aidha amesema kuwa upatikanaji wa nishati hiyo ni maendeleo kwa wananchi na viwanda, kwani Mkoa wa Kagera umekuwa na viwanda vingi, hivyo Wanakagera watautumia umeme huo kujiletea maendeleo
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, amesema tukio hilo ni la kihistoria kwa kuwa kusainiwa kwa mikataba hiyo kunamaanisha kuwa mikoa yote iliyokuwa nje ya gridi ya taifa sasa inakuwa na mpango wa kuunganishwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Razalo Twange, amesema lengo la tukio hilo lilikuwa ni kusaini mikataba miwili, hatua ambayo ni ya kihistoria na safari ndefu kwa TANESCO.