Dodoma FM
Dodoma FM
20 August 2025, 5:59 pm

Serikali kupitia PPRA imesema moduli hiyo mpya inalenga kuondoa changamoto zilizojitokeza awali na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mikataba ya umma, ili kuhakikisha thamani ya fedha na uwajibikaji vinaimarika.
Na Seleman Kodima.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Denis Simba, amesema changamoto mbalimbali katika usimamizi wa mikataba ya umma zimekuwa zikisababisha upotevu wa rasilimali, kupungua kwa thamani ya fedha na kuzorota kwa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya moduli mpya ya usimamizi wa mikataba ndani ya mfumo wa NeST, Simba amesema changamoto hizo ni pamoja na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi, ukosefu wa ufuatiliaji wa karibu, mabadiliko ya vifungu vya mikataba bila kufuata taratibu, na malipo yasiyoendana na kazi zilizotekelezwa.
Mafunzo hayo yamejumuisha taasisi mbalimbali za ununuzi yamelenga kuwajengea uwezo watendaji kutumia moduli mpya ya mfumo wa NeST. Washiriki wamesema mfumo huo umeongeza usawa na uwazi katika mchakato wa kuomba na kusimamia tenda za serikali.