Dodoma FM

Mgombea udiwani Tambukareli awaahidi wananchi kunufaika na fursa

20 August 2025, 5:46 pm

Picha ni Mgombea wa Udiwani kupitia chama cha Mapinduzi kata ya Tambukareli akiongea na wananchi mara baada ya kuchukua form. Picha na Julias Evarest.

Zoezi la Uchukuaji wa Fomu za uteuzi wa nafasi ya udiwani limeanza tangu Agosti 14 na linatarajia kwenda hadi Agosti 27 kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi agosti 28 mwaka huu.

Na Seleman Kodima.
Mgombea wa Udiwani kupitia chama cha Mapinduzi kata ya Tambukareli Clinton Manzi amewaahidi wakazi wa kata hiyo kufaidika na fursa zinazopatikana ndani ya kata hiyo pindi watakapo mpa ridhaa ya kuwa kiongozi katika eneo hilo.

Manzi ameyasema hayo baada ya kukabidhiwa fomu ya Uteuzi wa kugombea nafasi ya Udiwani na Msimamizi Msaidizi ngazi ya Kata ya Tambukareli ambapo amewaahidi wananchi wa eneo hilo kufaidika na taasisi zinazowazunguka pamoja na kufanikisha hali ya miundombinu ya barabara katika baadhi ya mitaa.

Sauti ya Clinton Manzi .

Wakati huo huo, Aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof Davis Mwamfupe amewataka wakazi wa kata hiyo kuongeza ushirikiano na kuhakikisha umoja wao unaendelea ili kufanikisha ushindi kwa chama hicho.

Hayo ameyasema baada ya hapo jana kukabidhiwa fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi ya udiwani ndani ya kata hiyo ambapo amewashukuru wananchi kuzidisha ushirikiano na umoja.

Sauti ya Prof Davis Mwamfupe.

Na Mgombea wa udiwani kata ya Zuzu (Nzinje), Bi Jenesta Project Malingo, amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo Agosti 19, 2025 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuahidi kuwaletea wananchi maendeleo yenye kasi, mshikamano na ushirikishwaji.

Bi Jenesta ambaye awali alikuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kata ya Zuzu, amesema wanachama wote wameunganishwa kwa lengo moja la ushindi wa CCM.

Mwenyekiti wa CCM kata ya Zuzu, Omari Bilali Kagusa, amesisitiza kuwa uchaguzi ndani ya chama ni jambo la kawaida na makundi lazima yafutwe mara tu mgombea rasmi anapopatikana.