Dodoma FM
Dodoma FM
4 August 2025, 4:15 pm

Ikumbukwe kuwa TADB inaadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa imewezesha wakulima kwa kutoa mikopo ya riba nafuu yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.129 katika kipindi hicho.
Na Seleman Kodima.
Imeelezwa kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aingie madarakani Ukubwa wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo TADB umeongezeka kutoka shilingi bilioni 362 hadi kufika kiasi cha trilioni 1.12 kwa Mwezi June mwaka huu 2025.
Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania TADB,Frank Nyabundege ameyasema hayo wakati wakielezea sababu za benki hiyo kuwa mdhamini mkuu wa Maonesho ya Sikukuu ya wakulima Nane Nane kitaifa yanayofanyika Jijini Dodoma.
Bw Nyabundege amesema ukubwa wa Benki hiyo umesababisha kuingia katika orodha ya benki kubwa nchini.
Amesema mchango wa Rais Samia katika Wizara za kisekta ni moja ya chachu katika sekta ya kilimo kutokana ongezeko la zaidi ya trilioni 2.8 hadi trilioni 4.55.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema mwaka huu wanasherekea miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Benki ya maendeleo ya Kilimo hivyo watakuwa na shughuli mbalimbali zitakazofanyika kutokana na benki hiyo kuwa mdhamini mkuu wa Maonesho ya Mwaka huu.
Hata hivyo Maadhimisho ya Nanenane ya mwaka 2025 yamebeba kauli mbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika kuchagua viongozi wanaojali maendeleo ya sekta hizi muhimu kwa uchumi wa taifa.