Dodoma FM
Dodoma FM
31 July 2025, 12:25 pm

Tukio hili limeibua maswali na mijadala mikali miongoni mwa wakazi wa mtaa huo, wakilalamikia ukosefu wa udhibiti wa vyombo vya usafiri katika maeneo ya makazi na hasa wakati wa shughuli za kijamii au sherehe.
Na Joseph Gontako
Katika tukio la kusikitisha lililotokea katika mtaa wa Chinangali kata ya Chamwino jijini Dodoma, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 7 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la kwanza, amejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na pikipiki (bodaboda) iliyokuwa ikiendeshwa kwa mwendo kasi wakati wa sherehe za kijamii zilizokuwa zikiendelea mtaani hapo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, bodaboda hiyo ilikuwa ikiendeshwa kwa uzembe bila kuzingatia hali ya mazingira, ambapo watu wengi wakiwemo watoto walikuwa wamekusanyika mtaani hapo kusherehekea harusi.
Dereva huyo wa bodaboda anadaiwa kupita katikati ya umati wa watu kwa mwendo wa kasi na bila tahadhari, hali iliyosababisha kumgonga mtoto huyo aliyekuwa akicheza pembezoni mwa barabara.
Mtoto huyo alikimbizwa kwa haraka katika Kituo cha Afya kwa ajili ya matibabu ambapo taarifa za awali zinaeleza kuwa anaendelea kupata huduma za kitabibu na hali yake inaendelea kufuatiliwa kwa karibu.
Tukio hili limeibua maswali na mijadala mikali miongoni mwa wakazi wa mtaa huo, wakilalamikia ukosefu wa udhibiti wa vyombo vya usafiri katika maeneo ya makazi na hasa wakati wa shughuli za kijamii au sherehe.
Wataalamu wa usalama barabarani wameendelea kusisitiza umuhimu wa elimu ya usalama kwa waendesha bodaboda pamoja na kuweka utaratibu wa ulinzi na tahadhari wakati wa mikusanyiko ya kijamii. Pia, imependekezwa kuwa na walinzi wa mtaa au vikundi vya ulinzi shirikishi kila kunapokuwa na shughuli zinazovutia watu wengi hususan watoto.