Dodoma FM
Dodoma FM
12 July 2025, 9:38 pm

Kongamano hilo ni la pili kufanyika baada ya la kwanza kufanyika Jijini Dar es salaam.
Na Seleman Kodima.
MKUU wa Mkoa wa Dodoma,Rosemarry Senyamule,anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la amani la Mkoa la kujadili suala la amani kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba Mwaka huu.
Kongamano hilo linafanyika ikiwa ni kuunga mkono kauli ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati analihutubia Baraza la Eid kwamba suala la amani ameliacha kwa viongozi wa dini ili kuzungumza na jamii wanazoziongoza kupitia makongamano ya amani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma,Naibu Qadhi Mkuu na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Taifa,Sheikh Ali Hamisi Ngeruko amesema mada tano zinatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano hilo ikiwemo athari ya mitandao katika kuchangia kuharibika kwa amani au kuleta maendeleo katika jamii.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Karmely Assemblies of God,Dokta Evance Chande ameiasa jamii kutojaribu kwa namna yoyote kuivuruga amani kwa kuwa madhara yake ni makubwa na kuwaasa wanasiasa kufanya kampeni za kistaarabu zisizowachochea wananchi kuwa na hasira.

Mchungaji John Maliga wa Kanisa la EAGT na mlezi wa Kamati za Amani Mkoa wa Dodoma Maridhiano Tanzania,,amewaomba Viongozi wa dini kuwa kielelezo cha amani na mfano bora wa kuitangaza amani.
Kongamano hilo ni la pili kufanyika baada ya la kwanza kufanyika Jijini Dar es salaam limebeba kauli mbiu isemayo amani yetu,Taifa letu ambapo mada nyingine zitakazojadiliwa ni afya ya akili,mahubiri na mchango wa vyombo vya dola katika kuimarisha amani na usalama wanchi.