Dodoma FM

Mpango aagiza Tamisemi, Afya kutatua haraka changamoto za waganga wakuu

12 July 2025, 9:05 pm

Picha ni Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Waganga wakuu wa mkoa na Halmashauri unaofanyika jijini Dodoma.Picha na Seleman Kodima.

Amesema lengo kuu la Mpango huo ni kutoa Muelekeo kwa watumishi wa Afya ngazi ya Msingi kufanya Tafiti na kutumia matokeo ya tafiti katika kutatua changamoto,Kuboresha utoaji wa huduma za afya.

Na Seleman Kodima.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Isdor Mpango amesema serikali imejizatiti kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya zikiwemo za kifedha kwa kuendelea kutafuta njia za kuongeza Rasilimali fedha zitakazo gharamia huduma afya kwa Ufanisi.

Amesema Wakati Serikali inaelekea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wote,ni Muhimu Mamlaka za serikali za mitaa nchini kuhakikisha zinasimamia vyema ukusanya wa mapato ili ziweze kutumika kuboresha utoaji wa huduma.

Dkt Mpango ametoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Waganga wakuu wa mkoa na Halmashauri unaofanyika jijini Dodoma ambapo ametoa maagizo mbalimbali kwa Wizara ya Tamisemi na Afya kuhakikisha wanashughulikia changamoto zinazowakabiliwa wataalamu hao.
Makamu wa Rais amesema serikali kwa kushirikiana na wadau wanafanya mapitio katika mfuko wa afya ili kuhakikisha fedha hizo zinapatikana kwa wakati.

Wakati Serikali inaelekea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Bima ya Afya kwa wote,ni Muhimu Mamlaka za serikali za mitaa nchini kuhakikisha zinasimamia vyema ukusanya wa mapato.Picha na Seleman Kodima.

Kwa upande Mwingine Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Philip Mpango amewahakikishia waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri kushughulikia changamoto walizoanisha katika Risala yao ikiwemo suala la Posho ya madaraka kwa waganga wafawidhi ambapo amewaagiza Mawaziri wa Wizara ya Tamisemi na Afya kuhakikisha wanatatua haraka.

Awali Waziri wa ofisi ya Rais ,Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa,Mhe Mohamed Mchengerwa amesema katika kuimarisha huduma za afya nchini ,Wizara hiyo kwa kushirikina na wizara ya Afya na UNICEF wameanda Mpango wa uimarishaji uwezo wa kufanya na kutumia tafiti zakiutekelezaji katika kuboresha huduma za afya ngazi ya Msingi kwa mwaka 2025-2030.

Nae Wazara wa Afya Mhe Jenister Mhagama amesema wameanza kufanyia kazi baadhi ya changamoto kwenye kada hiyo ikiwa ni pamoja Posho ya madaraka,Kuwajengea Uwezo Viongozi katika Sekta ya Afya,kuimarisha huduma ya dharura hapa nchini ili kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko.

Picha ni waganga wakuu wa mikoa wakiwa katika mkutano wa mwaka wa Waganga wakuu wa mkoa na Halmashauri unaofanyika jijini Dodoma.Picha na Seleman Kodima.

Mapema akiwasilisha Risala kwa Mgeni Rasmi,Mwenyekiti wa Waganga wakuu wa Mikoa Dkt Besti Magoma aliwasilisha baadhi ya Mapendekezo ikiwa ni sehemu ya kuongeza ushiriki wa pamoja wa sekta hiyo katika kukabiliana na Magonjwa ya Mbalimbali,kutengwa kwa fedha za dawa ili kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko.

Mkutano huo uliobeba kauli mbiu isemayo Wajibu wa Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri katika kuimarisha ubora wa huduma za afya kuelekea bima ya afya kwa wote unafanyika kwa siku Tatu ambapo wataalamu hao watafanya tathimini na kutoka na Mapendekezo ya namna bora ya kuendelea kuzidisha juhudi za utoaji wa huduma za afya nchini.